MAWAZIRI WAPYA WASEMA HIVI!!!!

Mawaziri walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete , wametoa kauli zenye kuleta matumaini mapya, huku wakielezea changamoto zinazowakabili katika kazi hiyo muhimu ya kitaifa.Baadhi ya mawaziri wapya na naibu mawaziri, wakizigusia changamoto zinazozikabili wizara zao na namna ya kuondokana nazo.
Hata hivyo, mawaziri na naibu mawaziri wengine hawakuwa tayari kuzungumza na gazeti hili, badala yake waliahidi kutoa tamko rasmi baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam kesho.

Waziri mteule wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, alisema mara baada ya kuapishwa , anatarajia kuanza kazi kwa kukishughulikia kilio cha muda mrefu cha madaktari kwa kusikiliza ripoti ya kamati maalum iliyoundwa.
“Ipo kamati iliyohusisha wajumbe kutoka serikalini na madaktari ambayo ilikuwa ikiangalia changamoto zilizotolewa na madaktari wakati wa mgomo. Nitaisikiliza imekuja na maoni gani kisha kazi ianze,” aliahidi.
Aliongeza kuwa, kasi ya kuyatatua matatizo hayo itategemeana na uwezo wa bajeti ya serikali.
Suala jingine aliloahidi kulipa kipaumbele ni pamoja na Bohari ya Dawa (MSD) ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau wengi juu ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba usioridhisha .
“Kwenye hili tutaangalia upya utaratibu wa kusambaza dawa ili maeneo yote yaweze kufikiwa kwa muda na wakati, lakini pia mfuko wa Bima ya Afya nao tutauangalia kwa mapana yake ili uweze kukidhi matakwa ya wanachama wake wote,” alisema.

Naibu Waziri mteule wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kwa upande wake alisema moja ya kazi watakayoanza nayo ni kuangalia gharama za simu za mitandao ambazo zimekuwa zikiwaumiza watumiaji.
“Mteja anaweka vocha ya Sh. 2,000 kwenye simu yake anaongea kidogo tu fedha yote inaliwa, kwa kweli hili lazima tulitazame maana wanasema gharama zao wamezipunguza lakini mtumiaji anaumia,” alisema.
 wanatarajia kupanua zaidi mkonga wa Mawasiliano wa Taifa ili maeneo mengi nchini yaweze kufikiwa na huduma za mawasiliano.
Pia Makamba alisema wizara yake inatarajia kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na wataalamu wengi wa sayansi badala ya kutegemea watu wageni kutoka nje.
“Hapa tutakachofanya ni kuwafanya wanafunzi kupenda masomo ya sayansi kama masomo mengine, ili nchi iendelee lazima izalishe wanasayansi wapya wazalendo na msingi wa maendeleo ni sayansi inayotakiwa kuanzia ngazi ya chini,” alisema.
Kwa upande wa Kampuni ya Simu Nchini TTCL , Makamba alisema wanatarajia kuipa hadhi na heshima TTCL, kwa kuziangalia changamoto zake ambazo zinaifanya ibaki nyuma ya kampuni nyingine za simu.
Akizungumzia masuala ya kukwamishwa na bajeti Makamba alisema kikubwa ni wizara kutengeneza hoja za kuitetea kama ilivyofanya Wizara ya Ujenzi mwaka jana ambapo Waziri wake aliweza kupata bajeti ya Sh. Trilioni 1.4 baada ya kujitetea kwa hoja madhubuti.

Dk. H Mwakyembe ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na kuteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi alisema kwa kifupi kuwa, kwa sasa hawezi kuzungumza lolote mpaka atakapoapishwa.
“Najua unatamani kujua mikakati ya wizara yangu mpya niliyopelekwa lakini ndugu mwandishi nitafanya hivyo mara baada ya kuapishwa,” alisema na kukata simu.


Waziri mteule wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kaghasheki, alisema hawezi kuzungumza na mwandishi kwenye simu na kwamba yeyote anayetaka kumhoji amfuate ofisini.
“Kwanza sijaapishwa na pia siku hizi kuna wajanja wengi, wanajitambulisha kwenye simu kuwa ni waandishi kumbe sio, tafadhali njoo ofisini kwangu tutaongea,” alishauri.

Waziri mteule wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, alisema baada ya kuteuliwa anasubiri kuapishwa ili kuanza kazi rasmi.
Wadau wengine waliozungumzia Baraza Jipya la Mawaziri ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe, ambaye kupitia mtandao wake, alisema juhudi za kurejesha misingi ya uwajibikaji katika utumishi wa umma zimeanza kuzaa matunda.
Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alimpongeza George Mkuchika , kwa kuwa mtulivu asiyekuwa na makuu wala kujitetea kama mawaziri watuhumiwa wengine.
Mkuchika amemrudisha kwenye baraza jipya kuwa Waziri wa Utawala Bora.
Aliwaonya mawaziri wateule juu ya kusherehekea uteuzi wao “Kwa kawaida wateule hufanya sherehe, nitawashangaa watakaofanya sherehe safari hii kwani hakuna cha kufurahia, nitawashangaa watakaoenda kuapa kwa maua kwani furaha itakuwa ya muda mfupi tu” ilisema sehemu ya safu hiyo na kuongeza:
“Mkutano wa Bunge wa Bajeti ni mwezi ujao tu na wateule wote watakuwa kikaangoni, Too short honeymoon, hakuna cha kusherehekea kwa sababu nchi inachangamoto nyingi” iliongeza.
Aliwaambia kuwa kazi iliyopo ni kuzalisha umeme wa kutosha na kuusambaza kwa wananchi wengi, kukuza uchumi wa vijiji na uzalishaji viwandani ili kutengeneza ajira kwa vijana. alitoa changamoto nyingine kuwa ni pamoja na kuongeza mapato ya utalii kutoka katika hifadhi za taifa na kuvutia watalii.
“Nimewapigia simu wateule wengi na kuwaambia siwapi pongezi bali nawatakia kazi njema na uwajibikaji kwa sababu ndio msingi wa kupambana na rushwa, uvivu na uzembe,” ilisema safu yake.
Kabwe ambaye ni Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi katika mtandao wake alimwambia Waziri mteule wa wizara hiyo, Dk. William Mgimwa, kuwa uteuzi wake ni changamoto kubwa katika maisha yake.
“Eneo lenye bajeti kubwa kuliko zote ni huduma kwa deni la taifa lazima kuangalia upya deni hili, kwa sasa ukilijumlisha na dhamana za serikali limefikia Shilingi tilioni 22 hadi Desemba mwaka 2011,” alisema na kuongeza:
“Nimewahi kutaka ukaguzi maalum katika ‘account’ ya deni la taifa. Ninarejea wigo huu, tunalipa takriban Shilingi tilioni 1.9 kwa mwaka ambayo ni zaidi ya bajeti ya miundombinu, afya, maji na umeme.”
Alimkumbusha Dk. Mwakyembe kuwa atakumbukwa iwapo ataimarisha na kuufanya usafiri wa reli ufanye kazi.
Aidha, alisema nchi inatumia Shilingi bilioni 300 kwa mwaka kukarabati barabara wakati inahitaji Shilingi bilioni 200 kukarabati reli kusafirisha mizigo kwenda na kutoka bandarini.

No comments:

Post a Comment