KIFO CHA KANUMBA CHA WEKA WENGI MATATANI


BADO sakata la kifo cha Steven Charles Kanumba ‘The Great’ ni bichi na kwa mambo yalivyo, kuna uwezekano watu wengi zaidi wakaingia matatani kwa namna moja au nyingine.
Habari zinadai kuwa wakati upelelezi ukiendelea, kuna ambao tayari wamehojiwa na inawezekana wengi watahojiwa kwa kadiri ishu hiyo inavyozidi kuchukua sura mpya.


Ukimwondoa mtuhumiwa namba moja wa kifo hicho, Elizabeth Michael ‘Lulu’, ambaye alishahojiwa na kupandishwa kizimbani kisha kuwekwa nyuma ya nondo za mahabusu ya Segerea, Dar, kuna wengine walio roho juu.
   
Katika tukio hilo, pia tayari ndugu ambaye ni mdogo wa marehemu Kanumba, Seth Bosco naye alishafikishwa kwenye kituo cha polisi cha Oysterbay Kinondoni na kuhojiwa kuhusu anachokijua juu ya kifo hicho kwa kuwa ndiye mtu wa kwanza kuingia chumbani baada ya staa huyo kudondoka.

 Naye aliyekuwa daktari wa marehemu Kanumba aliyetajwa kwa jina moja ka Kabugi maarufu kama Kidume, alikuwa mmoja wa watu waliofika kituo cha polisi Oysterbay kutoa maelezo akiwemo mwigizaji swahiba wa marehemu Kanumba, Vincent Kigosi ‘Ray’.
   
Pamoja na kuwa mmoja wa watu waliokwenda kutoa maelezo polisi siku ya tukio la kifo cha Kanumba Aprili, 7, mwaka huu, mwishoni mwa wiki iliyopita Ray alizua gumzo baada ya kupamba ukurasa wa mbele wa gazeti moja litokalo kila siku akikanusha kuhusika na kifo hicho.
Swali kwa Ray lilikuwa hivi.ni nani aliyemwambia kuwa kahusika hadi akanushe hivyo kumjengea picha ya tofauti kwenye jamii.

 Mwishoni mwa wiki iliyopita, staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba, naye alisikika akikanusha kuwa si kweli kwamba alihojiwa juu ya sakata hilo kufuatia madai kuwa ndiye aliyempa lifti Lulu wakati anaondoka kwa Kanumba baada ya tukio hilo.

 Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kindoni, Charles Kenyela alipokuwa akifunga mjadala huo na kuachia Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai kifanye kazi yake, katika sakata hilo watu wengi watahojiwa kwani watafuatilia vyanzo mbalimbali ikiwemo simu za Kanumba na Lulu kujua watu waliowasiliana nao wahojiwe wanahusikaje na tukio hilo.

Mbali na kesi ya mauaji ya Kanumba, pia waliotumia kifo cha Kanumba kujitajirisha (kufa kufaana) kwa kuchuuza bidhaa mbalimbali za msanii huyo mkubwa ndani na nje ya nchi, nao wameingia matatani kwa kukamatwa na kutiwa mbaroni.
Bidhaa ambazo zilipigwa marufuku kuuzwa na shirikisho la filamu nchini (TAFF) ni pamoja na nguo, vitabu na mikanda ya mazishi ya Kanumba hivyo kila aliyekamatwa na ‘prodakti’ hizo aliingia matatani.


Na Hivi Ndivyo Vipimo vya Marehemu Kanumba kutoka kwa Madaktari


MCHORO wa mfano unaoonesha jinsi kifo cha msanii wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba alivyokufa kutokana na tatizo la kutikisika kwa ubongo wake unawekwa hadharani kwa mara ya kwanza na Amani.
Kwa mujibu wa mchoro huo unaopatikana katika mtandao, unaonesha kitaalamu hatua kwa hatua jinsi ubongo unavyotikisika hadi binadamu kufikia hatua ya kukata roho.



Kitaalamu, tatizo lililompata marehemu Kanumba linaitwa ‘Brain Concussion’ ambapo ubongo ulihama kutoka kwenye makazi yake na hivyo kusababisha mfumo wa kupumua kushindwa kufanya kazi inavyotakiwa.


Kwa mujibu wa maelezo ya kitaalamu, mara nyingi hali hiyo husababishwa na mtu kuangukia kichwa, hasa sehemu ya nyuma kama siyo kula au kunywa kitu chenye madhara mwilini.

Wataalamu wanasema binadamu anapotokewa na hali hiyo hushindwa kuingiza hewa ya oksijeni (cardio-respiratory failure).

Cha kwanza, kwa mujibu wa madaktari, mara baada ya mtu kukutwa na hali hiyo, kucha zake hubadilika rangi na kuwa za bluu huku mapafu yakivilia damu na kuonekana kama maini.

Hatua nyingine ni mhusika kutokwa na povu kinywani muda mfupi kabla ya tukio la kukata roho kumfika.

Kwa kawaida,watalaamu wanasema, ili kujiridhisha kama tatizo ni hilo, madaktari hukagua ubongo ili kuona kama umevimba au kushukia kwenye uti wa mgongo jambo ambalo linadaiwa kutokea kwa marehemu Kanumba.



Habari zaidi zinasema kuwa, madaktari waliomfanyia uchunguzi wa saa 3 Kanumba, walichukua sehemu ya maini na majimaji ya machoni na kuvipeleka kwa mkemia mkuu wa serikali ili kubaini endapo marehemu alikula kitu chenye sumu.



Huku mkemia mkuu wa serikali akiendelea na uchunguzi huo, mitaani wadau na wapenzi wa marehemu wamekaa mkao wa kula wakisubiri kwa hamu majibu hayo, hasa kutokana na ukweli kwamba bado maneno ya mitaani yanapishana kuhusu ukweli wa kifo hicho.

Licha ya kwamba kesi ipo mahakamani lakini baadhi ya watu wanasema serikali ichunguze kwa undani sakata hilo kwa vile kuna uwezekano mkubwa kifo cha Kanumba kikawa na mikono mingi.

Kanumba alifariki dunia Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Sinza ya Vatican City Hotel kwa kile kilichoelezwa kutokana na ugomvi baina yake na mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

Marehemu alizikwa Aprili 10, 2012 katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Lulu alikamatwa na kuhojiwa na askari wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar kutokana na kifo hicho na baadaye kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Kisutu, Dar ambapo alisomewa mashitaka.

Kesi yake itatajwa tena Aprili 23, mwaka huu katika mahakama hiyo na yuko mahabusu ya Segerea.

 

No comments:

Post a Comment