Mario Balotelli nyota wa soka nchini Italia ambaye pia ni mchezaji
mweusi wa Klabu ya Manchester City ya Uingereza amesema ataondoka
uwanjani endapo atakejeliwa kutokana na rangi yake wakati wa mchuano wa
kombe la Mataifa Ulaya katika nchi za Poland na Ukraine mwezi Juni.
Matamshi yake yanatokea kufuatia makala ya BBC ambayo yaliangazia
ghasia katika viwanja vya soka kutokana na ubaguzi wa rangi katika nchi
hizo mbili.
Makala hayo yalionyesha mashabiki wakizungu wakiwakejeli wachezaji
weusi na kuwashambulia mashabiki wenye asilia tofauti na kizungu.
Wanasiasa na maafisa wa soka kutoka nchi hizo wamesema tatizo hilo limetiwa chumvi.
Kukejeliwa kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya Balotelli nchini Italia
mwaka 2009 kulifanya shirika la soka Ulaya UEFA kuweka sheria ya
kuwalazimisha marefa kusimamisha mechi ikiwa kejeli za ubaguzi wa rangi
zitaendelea.