ZITTO AAMSHA BALAA

Zitto aamsha balaa,Atoboa yalipokwa kinyemela kwenye Muungano Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), Zitto kabwe, amefufua hoja ya nafasi ya mafuta na gesi kuwa mambo ya Muungano na amesema bila kumung’unya maneno kuwa suala hilo kuendelea kubakia kama lilivyo, ni kuendeleza makosa.
Zitto ambaye pamoja na wabunge wenzake walikuwa Uholanzi kwa ziara ya kujifunza jinsi nchi hiyo inavyoendesha sekta ya mafuta ya petroli na gesi na kurejea hivi karibuni, ameandika makala ndefu kuhusu mafuta na gesi kuwa mambo ya muungano na kuipa kichwa cha habari “Mafuta kuwa suala la Muungano tulikosea.”
Kwa kauli yake, Zitto amesema kuwa ni dharau kwa Wazanzibari kuwaambia kuwa mafuta na gesi ni masuala ya Muungano wakati hakuna uwazi jinsi suala hilo lilivyoingizwa katika orodha hiyo, licha ya serikali kuwa na majibu mepesi.
“Katika moja ya vikao vya Bunge katika Bunge la Tisa, aliyekuwa Naibu wa Waziri wa Nishati na Madini Ndugu Adam Malima alileta kumbukumbu za mjadala Bungeni (Hansard) za mjadala wa suala la mafuta na gesi ili kuthibitisha kwamba jambo hili halikuuingizwa kwenye Katiba kinyemela,” alisema Zitto katika makala hiyo aliyoiweka kwenye ovuti yake jina la zittokabwe.wordpress.com.
Amesema wakati Muungano unaanzishwa mwaka 1964 mafuta na gesi hayakuwa masuala ya Muungano na kwamba baada ya kueangalia katika Hati ya Muungano ambayo ilikuwa ni sehemu ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1965, suala hilo halikuwamo katika orodha ya mambo 11 ya Muungano.
“Nyaraka nilizoziona zinaonyesha kwamba suala la mafuta na gesi asilia liliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano mwaka 1968.
Kuna watu wanahoji kihalali kabisa kwamba nyongeza ya jambo hili ilifanywa bila kufuata taratibu na hivyo kufanywa kinyemela na kuna wengine wanasema jambo hili lilifuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kupigiwa kura na Bunge la Muungano na kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge kutoka pande zote za Muungano,” anasema.
Hata hivyo, Zitto anafafanua kuwa wakati umefika kwa watafiti wa masuala ya Muungano kupekua nyaraka hizo na kusema ukweli  namna suala la mafuta na gesi lilivyoingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Alisisitiza kuwa  jambo hilo sasa ni  la Muungano kwa mujibu wa Katiba na ni dhahiri kuwa Watanzania wa Wazanzibari hawafurahishwi nalo na hivyo kuazimia kupitia Azimio la Baraza la Wawakilishi kwamba jambo hilo liondolewe kwenye orodha ya masuala ya Muungano, ameshauri kuwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapaswa kutoa uamuzi wa mwisho utakaomaliza mjadala huu.
Zitto katika makala hito amesema kuwa licha ya Bunge la Muungano kuamua kuongeza suala la mafuta na gesi asilia katika masuala ya Muungano, mwaka mmoja baada ya uamuzi huo liliundwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano (establishment order).
“Shirika hili halikuanzishwa kwa Sheria ya Bunge au kwa Sheria ya Makampuni kama yalivyo Mashirika mengi ya Umma hapa nchini bali kwa amri ya Rais … Katika amri hii ya Rais, Shirika la TPDC halikupewa ‘mandate’ (mamlaka ) ya kimuungano.
Shirika hili mipaka yake ilianishwa kuwa ni Tanzania Bara peke yake. Hivyo suala la Muungano likawekewa Shirika la Tanganyika kulisimamia!” Zitto anabainisha katika makala ndefu kuwahi kutolewa na Mbunge huyo tangu suala la mafuta na gesi litikise nchi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Mbunge huyo ambaye mwaka 2007 alipata kuamsha moto mkubwa juu ya kampuni za madini ya Barrick kushirikiana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kusaini mkataba wa mgodi wa Buzwagi ughaibuni, alisema TPDC imekuwa ikifanya kazi ya kusimamia sekta ya mafuta na gesi ikiwemo kutoa vibali vya kutafuta mafuta, kuingia mikataba na makampuni ya kimataifa na kuisimamia mikataba hiyo.
Alitaja miongoni mwa mikataba hiyo ni kwenye maeneo ambayo kama isingekuwa Muungano yangekuwa ni maeneo ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kwamba mbaya zaidi mikataba yote ya utafutaji na uchimbaji mafuta inafanywa inaingiwa na Waziri wa Nishati na Madini Wizara ambayo siyo ya Muungano.
“Hakuna hata eneo moja ambalo taratibu zimewekwa kwamba pale ambapo eneo hilo ni eneo lilikuwa chini ya himaya ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar basi mikataba isainiwe na Mawaziri wawili wa sekta hiyo kutoka kila upande wa Muungano,” anabainisha katika makala hiyo.
Zitto ametoboa siri katika kakala hiyo akisema kuwa miaka ya mwanzo ya 2000 TPDC iliingia mikataba ya vitalu kadhaa vya mafuta miongoni mwake ni nambari  9, 10, 11 na 12 mashariki ya visiwa vya Pemba na Unguja, pia Shirika hilo na Wizara ya Nishati waliingia mkataba mwingine katika kitalu kilichopo kati ya Pemba na Tanga (mahala ambapo kumekuwa na dalili za wazi za kuwapo mafuta kutokana na kuonekana kwa ‘Oil sips’ mara kwa mara.
“Vitalu 9, 10, 11 na 12 vilipewa kampuni ya Shell ya Uholanzi na kitalu cha kati ya Tanga na Pemba walipewa Kampuni ya Antrim ya Canada ambayo baadaye waliuza sehemu ya Kampuni yao kwa Kampuni ya RAK Gas kutoka Ras Al Khaimah huko United Arab Emirates.
Kwa kuwa Vitalu hivi vipo katika eneo la iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kabla ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikataa shughuli zozote kufanyika mpaka suala la Mafuta na Gesi kuondolewa katika orodha ya Mambo ya Muungano lipatiwe ufumbuzi,” ametoboa.
Alisema uamuzi wa Serikali ya Zanzibar ungechukuliwa na Serikali yeyote ile yenye mapenzi ya dhati na watu wake.
“Uamuzi huu ulileta mjadala mpana sana katika masuala ya Muungano na ambao hawana taarifa waliubeza sana.
Hata hivyo suala hili likafanywa ajenda katika vikao vya masuala ya Muungano vinavyoitwa Vikao vya Kero za Muungano. Miaka kumi suala hili linajadiliwa na Maamuzi hayafanyiki! Hivi sasa kila suala lenye kuangukia kwenye Katiba husukumwa huko na hivyo kutoa ahueni kwa wanaogopa kufanya maamuzi,” amesema.
Zitto ameshauri kuwa kwa hali ilivyo sasa mambo makuu mawili yafanyike kuhusu sekta ya mafuta; “ushauri wangu ni kwamba; kwa maana ya kuandikwa kwenye Katiba mpya ni kwamba suala la mafuta na gesi asilia liendelee kuwa suala la Muungano kwenye eneo la usimamizi wa Tasnia na leseni za utafutaji (Upstream Regulatory mechanism).
Hili ni eneo linalohitaji usimamizi wa dhati kabisa na kwa pamoja pande mbili za Muungano zinaweza kufanya vizuri zaidi.”
Pili, ananshuri kuwa: “Eneo la Uchimbaji na hasa kugawana mapato ya mafuta na Gesi (Profit Oil) lisimamiwe na kila upande wa Muungano kivyake.
Biashara ya Mafuta isiwe jambo la Muungano na hivyo kila Upande wa Muungano uwe na shirika lake la mafuta na gesi ambalo litashiriki kama mbia wa mashirika ya kimataifa katika uchimbaji, usafirishaji na uuzaji wa mafuta na gesi asilia.
Mapato yanayotokana na Mafuta (Profit Oil) na kodi nyingine zote isipokuwa mrahaba (royalty) yawe ni masuala yanayoshughulikiwa na Serikali ya kila upande wa Muungano kwa mujibu wa Sheria ambayo Serikali hizo zimejiwekea.”
Zitto amesema kuwa kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa gesi iliyogunduliwa ikiwa na ujazo wa futi trilioni 20; huku Msumbuji ikiwa na futi za ujazo trilioni 107, Angola chini ya futi za ujazo trilioni 100, Algeria futi za ujazo trilioni 100 na Nigeria ikiwa inaongoza kwa kuwa na futi za ujazo trilioni 189; ikiongoza barani Afrika. Kwa utajiri huo, anasema haitawezekana kuacha suala mafuta na gesi bila ufumbuzi katika mvutano wa Zanzibar na Tanzania bara.

No comments:

Post a Comment