Salma Hamidu, mkazi wa Igogo, jijini Mwanza ameibuka na kudai
amezaa na marehemu Steven Kanumba mtoto wa kike aitwaye Treasure Steven
Charles Kanumba (2), Ijumaa linashuka na maneno ya kinywa chake.
Alidai alianza
kufahamiana na marehemu mwaka 2006 wakati yeye akiwa kwenye Kundi la
Nyakato Arts chini ya Mwalimu Joseph.
Salma akasema kuwa, uhusiano wao uliunganishwa na Mwalimu
Joseph ambaye alimpa marehemu namba zake za simu wakati alipopeleka
filamu za Machozi Yangu na Siri Yangu kuifanyia uhariri (editing) jijini
Dar es Salaam katika studio alizokuwa akifanyia kazi marehemu.
“Marehemu alipoona picha zangu kwenye filamu hizo alivutiwa na
mimi katika kuigiza, akaomba namba zangu za simu kwa Mwalimu Joseph,”
alisema Salma.
Mrembo huyo aliendelea kuweka wazi kuwa, baadaye Mwalimu Joseph
alirejea Mwanza na kumtaka radhi kwa kumwambia alimpa Kanumba namba
zake za simu.
“Baada ya wiki mbili nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha ni Kanumba. Aliuliza kama huwa nasafirisafiri.
“Nilimjibu si sana kwa sababu nasoma. Wakati huo nilikuwa
nasomea kompyuta kwenye Chuo cha English Kingdom Nyakato,” alisema
Salma.
Akaongeza: Marehemu alinielewa, lakini akaniomba niwe mwenyeji
wake punde atakapokuja Mwanza, nikaridhia ombi lake, alikata simu,
lakini tukaendelea kuwasiliana kwa simu kila mara.
Salma alisema mawasiliano yake na Kanumba yalidumu kwa mwaka mmoja bila kuonana ‘laivu’.
Aidha, alidai kuwa siku moja marehemu alimpigia simu akimtaka
kujiunga na kundi lake lililopo Dar, akamkubalia lakini tatizo likawa
umbali. “Lakini marehemu akaniambia nisiwe na wasiwasi kuhusu hilo,”
alisema Salma.
Akizidi kumwaga data za uhusiano wao ulivyoanza, Salma alisema:
“Mwaka 2007, Kanumba aliniita Dar, alinitumia tiketi ya ndege
ya Precision Air, kwetu niliaga nakwenda kumsalimia mama mkubwa
anayeishi Tabata.
“Nilipofika Dar, nilimpigia simu Kanumba kumtaarifu nimefika,
akanitaka tukutane Ubungo Plaza Hotel (Blue Pearl),” alisema Salma.
Pale Ubungo Plaza, marehemu kwa mara ya kwanza alimtamkia
lililo moyoni mwake kwamba ametokea kumpenda na akamuomba wawe wapenzi.
“Sikuwa na uamuzi wa haraka, lakini kutokana na ushawishi wake nilikubali, baadaye nilirudi Tabata kwa mama mkubwa.
“Usiku alinipigia simu, akaniomba kesho yake tusafiri kwenda
Zanzibar, nilikubali, asubuhi niliaga kwa shangaza tukaenda Zanzibar.
“Tulifikia Bwawani Hoteli. Tulikaa kwa siku tatu na kwa mara ya
kwanza nilikutana na marehemu kimwili. Tuliporudi Dar mimi nikarejea
Mwanza,” alisema Salma.
“Baada ya kama miezi minne na siku kadhaa hivi, marehemu
alinipigia simu akasema yuko Mwanza, anataka kuja chuoni kuniona.
Alikuja akiwa ameongozana na marafiki zake wawili, Credo na Theonist
Rutashoborwa.
“Walikuja hadi chuoni, mimi nilitoka tukaenda kukaa kwenye baa
ya Shentemba. Ilipofika saa 2 usiku, tukahamia Isamo Hotel,” alisema
Salma.
Salma aliendelea kusema kuwa, pale Isamo walipata chakula kabla
ya kujitupa kitandani lakini siku hiyo muda mwingi alikuwa akijisikia
vibaya, marehemu akamtaka asubuhi akapime.
“Asubuhi nilikwenda kwenye Kliniki ya Dokta Ng’walida, daktari
bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto. Vipimo vilionesha nilikuwa
na ujauzito wa miezi minne.
“Nilimwonesha marehemu majibu yale, hakuonekana kukubali wala
kukataa, lakini baadaye akasema kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala
familia hadi atakaponiambia.
“Baada ya siku mbili, aliaga kurejea Dar pamoja na marafiki
zake. Siku chache baadaye huku nyuma kwa bahati mbaya ujauzito ulitoka,
nilikwenda kwa daktari mmoja Nyakato National ambaye alithibitisha hilo.
Huo ulikuwa mwaka 2008.
Salma alisema kuwa mawasiliano na marehemu yaliendelea. Kuna siku alimpigia simu akimtaka wakutane jijini Arusha.
Alipofika alipokelewa na Kanumba mwenyewe kabla ya kwenda kupiga kambi kwa rafiki yake mmoja aliyekuwa akiishi peke yake.
Akasema kukutana kwao kimwili kwa safari hii, ndiko kulimpa ujauzito na hatimaye kujifungua binti anayeitwa Treasure au Tunu.
Arusha waliondoka na ndege hadi Mwanza ambapo walifikia Ladson
Hotel, ipo Bwiru na kukaa kwa siku mbili kabla ya kumruhusu kurejea
nyumbani kwao Igoma.
Akiwa na ujauzito huo, Kanumba alimtumia nauli akimtaka wakutane mjini Morogoro.
“Nikiwa na tumbo langu, aliniita Morogoro, nilisafiri kwa basi
hadi kule, nilifikia kwa shangazi yangu yeye alipanga kwenye hoteli ipo
jirani na Kituo cha Mabasi cha Msamvu.
“Kulitokea kutokuelewana kidogo na marehemu kwa sababu ya
ujauzito ule, akirejea mazungumzo yake ya awali kuwa, kazi yake
haimruhusu kuwa na mtoto wala familia, lakini nilimwambia sina namna ya
kufanya kuhusu ujauzito ule.
“Hata hivyo, marehemu alinionya nisimwambie mtu kuhusu ujauzito
kuwa ni wa kwake, iwe siri yangu na yake kwa sababu hakutaka habari
hiyo ifike kwenye magazeti,”alisema Salma.
Akaongeza: Baada ya hapo, alinipa shilingi 150,000 nikarudi nyumbani Mwanza.
“Nikiwa Mwanza alikuwa akinipigia simu akitaka kujua
naendeleaje na tumbo langu na kunitaka nijiandae kwa safari ya Dar,
atanitumia tiketi ya ndege.
“Nilisafiri, nilipofika Dar nilimjulisha, akasema tusikae Dar,
twende Zanzibar. Kule tulifikia tena Bwawani Hotel. Tulikaa kwa siku
nne, kisha tukarejea Dar.
Lakini tukiwa Zanzibar kuna mtu alinipigia simu na yeye
akiwepo, alikasirika sana na kuninyang’anya simu, akachukua namba kisha
akampigia mtu huyo, waligombana kwenye simu. Aliipasua simu yangu,
akaenda kuninunulia nyingine.
“Alikuwa mtu mwenye hasira, hakutaka kusikia unazungumza na
simu hasa ikiwa ni sauti ya kiume. Ugomvi huo ulisababisha aikane mimba,
akasema namsingizia ni ya mwanaume aliyenipigia simu. Ilifika mahali
akasema kila mtu aishi kivyake.
“Hata hivyo, alikuja kuniomba msamaha huku akizidi kunionya kuwa ole wangu nitangaze nina mimba yake.”
Alisema ugomvi wake na Kanumba ulitokana na ujauzito na ilifika
mahali Salma alimweleza mama yake ambaye alimlaumu kwa kujiingiza
kwenye uhusiano na mwanaume huyo.
Kwa upande wa misaada, Salma alisema akiwa mjamzito, marehemu
alimtumia shilingi Milioni mbili na laki mbili kwa ajili ya kununua
kiwanja.
Baadaye alimtumia shilingi Milioni moja za kupanga nyumba.
Fedha hizo alizituma kupitia Benki ya Standard Chartered Tawi la Mwanza.
Baada ya kutuma fedha hizo, marehemu aliwahi kwenda Mwanza na
kufikia kwenye Hoteli ya Ryans Bay. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wa
miezi saba.
Salma anasema: Nilimtaka tupige picha ya ukumbusho akakataa,
lakini nilipojifungua alikuja na kumpiga picha mtoto kwa kutumia simu
yake akisema, ‘mtoto mama yangu mtupu kwani amefanana naye sana.’
Aliongeza kuwa alipojifungua Kanumba alimtumia shilingi 500,000
za matumizi ya mtoto kupitia simu ya mama yake mzazi na Salma
(hakumtaja jina).
Aliendelea kusema kulijitokeza sakata wakati wa kumpa jina
mtoto, Kanumba akitaka amwite jina la mama yake, huku Salma naye akitaka
kumwita la mama yake, ndipo wakakubaliana mtoto aitwe Treasure au Tunu
ili kumaliza mzozo wa kugombea kumwita mtoto jina la upande mmoja.
“Treasure alipofikisha miezi saba alisema nimpige picha
nimtumie ili amwone alivyofikia, nilifanya hivyo. Siku moja akaniambia
angetunga filamu kuhusu maisha yetu ambayo alipendekeza iitwe My Gift.
“Siku chache kabla ya kifo chake alinipigia simu pamoja na
mtoto akisema alitaka kusafiri na asingekuwepo kwa mwezi wote wa Machi
mwaka huu, alimsalimia mwanaye. Lakini cha kushangaza siku chache
nikapewa taarifa za kifo chake,” alisema Salma.
Salma alisema mpaka sasa anashindwa kuelewa ni kwa nini
marehemu alitaka uhusiano wao uwe wa siri. Lakini baadhi ya marafiki
zake walikuwa wakifahamu uhusiano huo.
“Kanumba kaniacha njia panda, sijui la kufanya, lakini ni vyema
kama angemtambulisha mwanaye kwa ndugu zake kuliko hivi sasa ambapo
mengi yatazuka kuwa pengine natafuta fedha za marehemu.
“Sijaweka wazi ili nipate chochote, bali nahisi dhambi kuficha kwa sababu huyu mtoto si damu yangu peke yangu.
“Nitakuwa mbaya kwa Mungu kama nisiposema ukweli. Angekuwepo
mwenyewe nisingesema kwa sababu yeye ndiye alikuwa kiongozi wa maisha ya
mtoto.
“Narudia tena, nina uwezo wa kumlea na wala sihitaji mtoto
achukuliwe na kwenda kuishi kwa baba, ila familia ijue kuna damu yao
kwangu.
“Kama hawataamini, niko tayari kufika Dar na kupima DNA ili familia ya marehemu ijiridhishe,” alisema Salma.
Hata hivyo, Salma alikiri kufanya kosa la kutowahusisha
marafiki wa Kanumba kumtegulia kitendawili hicho na kudai pengine umri
mdogo ulichangia. Salma alizaliwa mwaka 1987.
Alisema mtu pekee ambaye watu wanamfahamu na ndiye shahidi wa
uhusiano wake na marehemu ni msanii wa maigizo, Ramadhan Malele ‘Swebe’
ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara.
Salma alisema kabla Kanumba hajafikwa na umauti, yeye aliwahi
kukutana na Swebe jijini Mwanza ambapo alimsimulia hali ilivyo na
akamshauri kusikiliza matakwa ya marehemu ya kutotoa siri ya kuwepo kwa
mtoto huyo.
No comments:
Post a Comment