Mawaziri 7 wajiuzulu wakiwemo Mkuchika na Ngeleja


Translation

Mawaziri saba wameandika barua za kujiuzulu nyazifa zao kwa kile kinachodaiwa ni shinikizo kutoka kwa wabunge wa Chama  cha Mapinduzi (CCM) ambao unatokana na udhaifu katika utendaji wao wa kazi.
Kwa mujibu wa vyanzo kutoka ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, kilichoketi katika ukumbi wa Piusi Msekwa mara baada ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge usiku, waliojiuzulu ni Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi),George Mkuchika na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel  Maige, Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe na  Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami.
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe akisaini karatasi inayokusanya saini za wabunge za kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa lengo la kuwasilisha kwa Spika mjini Dodoma. Kulia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto.
 
Hata hivyo,  imeelezwa kuwa hali hiyo imechochewa na taarifa zilizowasilishwa na Kamati mbalimbali za Bunge kati ya juzi na jana.Kamati zilizowasilisha ripoti zao juzi ni Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma POAC, inayoongozwa na Zitto Kabwe, Kamati ya Hesabu za Serikali PAC ya John Cheyo na ile ya Serikali za Mitaa LAAC, inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema.
Kamati zilizowasilisha ripoti zake jana zilikuwa ni pamoja na Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na Januari Makamba, Kamati ya Miundombinu inayoongozwa na Peter Serukamba na Kamati ya Fedha na Uchumi ambayo mwenyekiti wake ni Dk Abdallah Kigoda.
Kamati zote hizo zilikuja na ripoti kadhaa zilizoonyesha udhaifu katika utendaji hali iliyolazimisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, kuanzisha zoezi la kuandaa hoja ya kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ajiuzulu.
Hadi kufikia jana mchana wabunge 62 wakiwemo wa CCM, waliweka sahihi katika hoja hiyo inayotakiwa kusainiwa na wabunge wasiopungua 70.
Hali ndani ya Bunge imeanza kuwa ya moto kwa sababu matarajio ya Watanzania hajafikiwa na hakuna kiongozi wa serikali anayejali kuhusiana na hilo.
Katibu wa wabunge wa CCM, Jenister Mhagama jana usiku aliwaita waandishi wa habari katika ofisi za Bunge lakini hata hivyo hakukataa wala kuthibitisha kuandika barua za kujiuzulu kwa mawaziri hao.
“Wabunge wa CCM wametekeleza wajibu wao mkubwa wa kikanuni na kikatiba wa kuona namna gani wanaishauri serikali na maamuzi yaliyotokana na kikao chetu yatatolewa na viongozi waandamizi…kiongozi wetu mwandamizi aliyepo hapa Dodoma ni Mwenyekiti wetu (Mizengo Pinda),”alisema ikiwa ni muda mfupi mara baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuondoka katika ukumbi wa Pius Msekwa.
Licha ya waandishi wa habari kuhoji mara kadha kwanini amewaita usiku kama walikuwa hawajafikia hatua ya kusema maamuzi yao, Mhagama alisisitiza kuwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu msemaji ni mwenyekiti wa wabunge wa CCM na kwamba taarifa itatolewa kwa umma na Pinda.
Hata hivyo, Mhagama aliitaka serikali ijitathimini upya kuanzia kwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri hadi katika ngazi ya kijiji na kuchukua uamuzi.
Awali Spika Makinda, amesema zoezi linalofanywa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, (Chadema), Kabwe Zitto linalolenga kuwasilisha bungeni hoja ya kumwondoa waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni batili.
Makinda aliyasema hayo jana jioni wakati wabunge wakiendelea kuchangia ripoti za kamati mbalimbali zilizowasilishwa bungeni jana.
Alitoa maelezo hayo baada ya kuombwa mwongozo na Mbunge wa Bumbuli (CCM), Januari Makamba ambaye alitaka kufahamu kama zoezi hilo utaratibu ukoje.
Alisema azma ya kutokuwa na imani  na Waziri Mkuu imeelezewa katika kifungu cha 133 cha kanuni na kwamba imepewa nguvu katika katiba ibara ya 53 A kifungu kidogo cha tatu.
Alisema anafikiri Zitto alitaka kuwasilisha hoja hiyo, kwa sababu ibara ya  51 kifungu kidogo cha B kinasema Waziri Mkuu anateuliwa na  Rais lakini kabla ya kuwa waziri mkuu anaapishwa na Bunge.
“Naye hatashika madaraka yake hayo mpaka hapo uteuzi wake utakapothibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na wabunge walio wengi,”alisema.
Alisema ndio msingi wa Zitto kwamba huyo ni mtu waliyempitisha wenyewe na kwamba wabunge wanamamlaka naye kwasababu wamemthibitisha.
Alisema wakati huo huo ibara ya 52 ya Katiba  inatamka kuwa Waziri Mkuu ndiye atakayekuwa kiongozi wa shughuli za bunge bungeni.
Alisema kuwa vifungu vya Katiba vinafanana na kanuni za Bunge ambapo kifungu cha 53 ibara ndogo ya pili inasema serikali ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania chini ya mamlaka ya Rais, ndiyo itakayokuwa na itakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya sera ya serikali kwa ujumla.
“Mawaziri chini ya uongozi wa Waziri Mkuu watawajibika kwa pamoja bungeni kuhusu utekelezaji wa shughuli za serikali ya jamuhuri ya muungano hivi vifungu ndivyo vinatupa nguvu kwamba tunauwezo na waziri mkuu,”alisema.
Alisema lakini kifungu cha ibara ya 53 A na 63 ibara ndogo tatu kinaeleza kuwa wabunge hatapiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu ikiwa, “Taarifa ya maandishi iliyotiwa sahihi na kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote itatolewa kwa Spika angalau siku 14 kabla ya siku ambayo inatakiwa kuwasilishwa bungeni.”
Alisema kipengele B kinatamka kuwa Spika atajiridhisha kwamba masharti ya Katiba  kwa ajili ya kuleta hoja yametimizwa na kwamba masharti yenyewe yapo katika ibara ya 53 A kifungu kidogo cha pili.
Alikinukuu kifungu hicho kidogo cha pili kinasema bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii hoja yoyote ya kutaka kupitisha kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu haitatolewa bungeni ikiwa haina uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya waziri mkuu kwa mujibu wa ibara ya 52 ya Katiba.
Alifafanua kuwa katika kifungu hicho kidogo cha pili B kinasema  hoja hiyo haitatolewa bungeni ikiwa hakuna madai kwamba waziri mkuu amevunja sheria ya maadili ya uongozi wa umma.
Pia alisema kipengele C kinatamka kuwa hoja hiyo haitawasilishwa ikiwa haijapita miezi sita tangu ameteuliwa.
Alisema katika kipengele cha D kinaeleza kuwa kura hizo hazitapigwa ikiwa haijapita miezi tisa tangu hoja ya namna hiyo ipotolewa bungeni na mbunge na ikakataa kupitishwa.
Alisema la msingi hapo ni zile sahihi zinazotakiwa kuwepo, taarifa ipelekwe kwa spika kwa maandishi siku angalau 14 kabla ya siku inayokusudiwa kuwasilishwa.
“Sasa hiyo ya habari ya mheshimiwa wakati anachangia jamani njooni njooni hiyo utaratibu akitumia hiyo hiyo haikubaliki kwa sababu mimi sijapata hoja kabisa hadi sasa,”alisema na kuongeza:
“Maanake hili bunge linaahirishwa tarehe 23 maanake Jumatatu …haikidhi siku 14 sana sana anaweza kuzikusanya labda Bunge lijalo na zenyewe ziwe sio chini ya siku 14 kwa hiyo zoezi linaloendelea au kama linafanywa ni batili kwa maana hiyo,”alisema na kwamba siku tatu zilizobakia yatakuwa haina msingi

No comments:

Post a Comment