20%,AFANDE SELE HOI HOI HOI


 
VARANGATI kubwa limetokea ‘Mji Kasoro Bahari’ Jumanne iliyopita baada ya wananchi wenye hasira kuwapopoa kwa mawe wanamgambo wa manispaa kupinga kitendo chao cha kuwapa kichapo wasanii wa Bongo Fleva, Seleman Msindi ‘Afande Sele’ na Abbas Hamis Kinzasa ‘20%’,  
 Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, kabla ya mastaa hao kutandikwa virungu na wanamgambo hao wa manispaa, walitinga katika Benki ya Makabwela ya NMB Tawi la Wami saa 12:00 jioni wakiwa katika gari aina ya Toyota Stout lenye namba za usajili T 631 BAV wakiwa na nia ya kutoa fedha.

 Baada ya kushuka kwenye gari huku wakitembea kwa mikogo ya kisanii, Afande Sele na 20%, moja kwa moja walikwenda katika kichumba cha ATM ili kuchukua mikwanja yao kwa ajili ya kutumia.
Wakiwa ndani ya kichumba hicho cha ATM, wakihesabu fedha zao na kupanga matumizi, wanamgambo wa manispaa walifika na kuanza kulizunguka gari lao bila ya wao kuwa na habari.


 
Baada ya kulizunguka kwa dakika mbili tatu, wanamgambo hao waliridhika kwamba gari hilo lilikuwa limeegeshwa vibaya yaani kwa msisitizo wa Lugha ya Malkia walisema ‘wrong parking’, hivyo wakalifunga mnyororo.
Wakati wakifanya kitendo hicho, Afande na 20% walikuwa tayari wameshamaliza kuhesabu na kupanga matumizi ya fedha zao, wakasogea katika gari lao, ndipo walipowakuta wanamgambo wakiendelea na zoezi  hilo na kuwazuia hali iliyozua purukushani ‘


 Hali ilikuwa mbaya baada ya kuzuka mshikemshike kati ya mastaa hao na wanamgambo ambao waliongeza nguvu na kuanza kuwatandika mastaa hao kwa virungu ili kuwanyong’onyesha nguvu.
 
 Wananchi waliokuwa wakishuhudia tukio hilo, walipandwa na hasira kwa kuona kwamba Afande Sele na 20% walikuwa wakionewa, hivyo wakachukua jukumu la kuwapigia simu polisi ili kuripoti tukio hilo.
Kama vile haitoshi, wananchi hao wakaongeza hatua nyingine kwa kuamua kuwapopoa kwa mawe wanamgambo wa manispaa baada ya kuona askari polisi wasingeweza kuwahi kufika eneo la tukio.
Mmoja kati ya wanahabari wa blog hii, Alikutana na gari aina ya Toyota Land Cruser lililokuwa katika mwendo wa kasi likitokea kwenye kisanga hicho huku ndani yake kukiwa na wanamgambo na mastaa hao wakiwa wamedhibitiwa vilivyo.
Mbali na kuwa katika mwendo wa kasi, gari hilo lilionekana kuvunjwa kioo chake cha nyuma na wananchi waliokuwa na hasira waliokasirishwa na kitendo hicho walichokiita cha uonevu.
Mwandishi wa Kashaiblog akiwa na usafiri wake, alilifuatilia gari hilo hadi Kituo Kikuu cha Polisi cha Manispaa ya Morogoro ambapo wasanii hao walishushwa kwenye gari hilo huku wakivuja damu kutokana na kichapo kilichokuwa kikiendelea ndani ya gari.

 

Kichapo hicho kilimfanya Afande Sele kutoa maelezo huku akiwa anamwaga machozi kwa uchungu wakati mwenzake 20% akigugumia kwa maumivu aliyoyapata katika sakata hilo.
Baada ya kuchukuliwa maelezo, mastaa hao walitupwa mahabusu ambako walilala hadi Jumatano walipopelekwa Mahakama ya Mwanzo ya Mazimbu kujibu mashitaka matano.
Kati ya mashtaka hayo ni kuharibu mali, kuvunja kioo cha nyuma cha gari lenye namba za usajili SM 3323 aina ya Toyota Land Cruser chenye thamani ya shilingi laki nane.
Lingine ni kujeruhi, mlalamikaji akiwa ni Waziri Ramadhan na makosa mengine matatu ambapo kesi hiyo ilitarajiwa kuendelea tena jana Alhamisi.

No comments:

Post a Comment